5 Machi 2023 - 15:52
Rais Raisi: Iran inatarajia IAEA itakuwa na muelekeo wa 'kitaaluma, usio wa kisiasa'

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raeisi anasema Tehran inatarajia Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) utachukua mtazamo wa "kitaalamu" kuhusu mpango wa Iran wa nishati ya nyuklia na kujiepusha kuathiriwa na baadhi ya madola ambayo yanafuatilia malengo yao mahususi.

Katika kikao na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi mjini Tehran siku ya Jumamosi, Raisi amesema Iran imekuwa na ushirikiano wa hali ya juu na wakala huo kwa msingi wa nia njema  ya nchi hii.

Akiashiria mazungumzo ya Grossi na maafisa wa Iran mjini Tehran, rais huyo ameeleza matumaini yake kuwa IAEA itachukua hatua kwa kuzingatia mienendo ya kitaaluma na ya haki na kanuni ya kutoegemea upande wowote ili kutangaza ukweli kuhusu shughuli za amani za nyuklia za Iran na kuzingatia kanuni za nchi.

Amesema ziara za maafisa wa IAEA mjini Tehran zinaonyesha "azma thabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuwa na ushirikiano wenye manufaa na wakala huo."

Akisisitiza haja ya kutumia teknolojia ya nyuklia katika viwanda, kilimo na dawa ili kuboresha ustawi wa wananchi, Raisi amesema, "Baadhi ya nchi, zikiongoziwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinatumia kadhia ya nyuklia kama kisingizio cha kuwashinikiza zaidi watu wa Iran, wakati utawala wa Kizayuni haujakuwa mwanachama wa wakala na wala haufuati kanuni zake."

Rais wa Iran amesema Marekani ni mkiukaji wa kwanza wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, ambayo yanajulikana rasmi kwa jina la Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) kwa kujiondoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo.

Wakati  huo huo Naibu mkuu wa Ofisi ya Rais wa Iran katika masuala ya kisiasa, Mohammad Jamshidi, amesema katika chapisho kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba Grossi "ameelezea kuridhishwa na ajenda ya pamoja iliyoafikiwa ili kuandaa njia ya ushirikiano."

"Rais Raisi amesisitiza kuwa ushirikiano ni njia ya pande mbili ambayo msingi wake ni uhuru wa kujiamulia mambo IAEA huku haki za taifa la Iran zikizingatiwa," ameandika kwenye Twitter.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Mohammad Eslami mapema siku ya Jumamosi, Grossi alisema shambulio lolote la kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia ni marufuku. Kauli hiyo ilikuwa ya kujibu vitisho vya Marekani na Israel vya kutaka kulenga vituo vya nyuklia vya Iran.

Akiwa mjini Tehran Grossi pia amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian ambapo amesema  ni "suala la lazima kuwa na mazungumzo ya kina na Iran."


342/